Tuesday 1 August 2017

Filled Under:

MBIO ZA MWENGE WILAYANI BUHIGWE 2017

                 Mbio za mwenge wa uhuru wilaya  ya Buhigwe kwa mwaka 2017 zilifanyika tarehe   27-28/07/2017   wilayani hapa, ambapo Jumla ya miradi saba (7) yenye thamani ya shilingi.1,946,132,975 imetembelewa na mwenge wa uhuru mwaka huu 2017 na kuzinduliwa/kuweka jiwe la msingi.
Ndg Frederick Joseph Ndahani (mkimbiza mwenge kitaifa) akikimbia na mwenge wa uhuru  Kata ya Kinazi wilayani Buhigwe  


 Aidha, Serikali kuu imechangia shilingi 1,819,532,975 sawa na 94% Halmashauri shilingi 14,200,000 sawa na 1%, Wahisani shilingi 87,000,000 sawa na 4% na Wananchi shilingi 25,400,000 sawa na 1% katika kufanikisha uzinduliwaji wa miradi hiyo.

Mbali na uzinduzi wa miradi hiyo, mbio za mwenge kwa mwaka 2017 zilibeba jumbe nne (4) kuu kuwafikishia wananchi


  • "MADAWA YA KULEVYA" Mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, tuwajali na kuwasikilize watoto na vijana.
  • "RUSHWA" Tuungane kwa pamoja dhidi ya rushwa kwa maendeleo, amani na usalama wa Taifa letu.
  • "UKIMWI" Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI inawezekana ifikapo mwaka 20130
  • "MALARIA" Shiriki kutokomeza Malaria kabisa kwa manufaa ya jamii.
Miradi ambayo mwenge wa uhuru kwa mwaka 2017 ilizindua wilayani Buhigwe ni kama ifuatavyo:
  1. Mradi  wa maji Katika kijiji cha Kirungu. Ujenzi wa miundo mbinu ya Maji ya  bomba katika Kijiji cha Kirungu unaendelea kujengwa na  Mkandarasi mjenzi  KAM / JUVE CONSTRUCTION LTD, ukisimamiwa na wataalamu wa maji toka ofisi ya mhandisi wa maji Wilaya ya Kasulu na Buhigwe. Lengo kuu la Mradi ni kuwapatia wananchi wa Kirungu  huduma ya maji safi na salama na ya kutosha kwa umbali  usiozidi mita  400 toka majumbani mwao kwa kuzingatia sera ya maji ya mwaka 2002, kwa kufanya hivyo wananchi  watapata muda wa ziada wa kufanya kazi nyingine za uzalishaji  mali na kujiletea maendeleo. Katika  mradi huu kazi zifuatazo  zimefanyika; ujenzi wa chanzo cha maji umekamilika kwa asilimia 95 , ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye  mita za ujazo 150m3 unaendelea na umefikia asilimia 85, njia kuu ya bomba (4,081m)  imekamilika kwa  asilimia 85,njia za mitawanyo kijijini (5,709m) imekamilika kwa  asilimia  90 na Vituo vya kutekea maji 15 (double type taps) vimejengwa na kukamilika kwa  asilimia  80. Mradi wa maji wa Kijiji cha Kirungu utakapokamilika utagharimu kiasi cha Tshs 504,788,762 (Wananchi  Tsh3,200,000/=, Halmashauri Tsh 4,000,000/= na Serikali kuu Tsh 497,588,762)mpaka kufika hatua hii mkandarasi ameishalipwa kiasi cha Tshs 412,839,702.20 na chanzo cha fedha hii  ni serikali kuu.
    Ndg Amour Hamad Amour akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji kijiji cha KIRUNGU
     
  2. Klabu ya Wapinga  rushwa  -Shule ya Sekondari  ya  Saint  Mathias Mulumba. Klabu  ya wapinga rushwa ya shule ya Sekondari Saint Matius  imeanzishwa mwaka 1994 ikiwa ni sera ya Serikali ya kuwajenga vijana kimaadili. Klabu hii ina jumla ya wanachama 40 waliojiunga kwa hiari yao wenyewe na wamepewa mafunzo kuhusu maana ya rushwa, aina za rushwa, sababu na madhara ya rushwa kwa Taifa letu. Klabu hii ni miongoni  mwa klabu kumi na tisa (19) za  shule za msingi na sekondari ambazo zimeshaanzishwa katika Wilaya ya Buhigwe. Lengo kuu la kuanzishwa klabu hii  ni  kuelimisha jamii kuhusu maana ya rushwa,  madhara  na umuhimu wa kuzuia na kupambana na rushwa. Wanafunzi wataelimisha jamii kwa njia ya midahalo, michoro, nyimbo, ngonjera, mashairi, maigizo na makala ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU. Kazi zinazotekelezwa ni kutoa mafunzo kwa Vijana kwani ni rasilimali muhimu katika kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuwa ni  wepesi wa kujifunza na kubadilika. Wakishirikishwa ipasavyo katika mapambano dhidi ya rushwa tutajenga jamii ya Watanzania waadilifu ambao wataichukia rushwa na maovu yote na hivyo kuleta maendeleo. Hili litakuwa suluhisho la uhakika na la kudumu katika kuikabili rushwa kwani mmomonyoko wa maadili ni moja ya sababu za msingi za kuwepo kwa rushwa katika jamii.
    Ndg Amour Hamad Amour, azidindua mradi wa wapinga rushwa katika shule ya sekondari ya mtakatifu Mathius Mulumba iliyopo Janda
  3. Ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya  Buhigwe. Ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi  makao makuu  Wilaya ya Buhigwe umeanza mwaka 2015  ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwa  na ofisi  za utawala  katika makao  makuu ya wilaya

    Halmashauri imepokea kiasi cha Tsh 1,200,000,000/= (Tsh 450,000,000/= kwa mwaka 2014/15 na Tsh 750,000,000/= kwa mwaka 2016/17) kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu. Mradi huu unatekelezwa naTanzania  Building  Agency  (TBA)  ambayo ni taasisi ya Serikali. Lengo kuu la mradi  huu  ni   kuboresha mazingira ya kiutendaji kazi  ya  kiutawala   na   kitaalamu. Aidha, Ujenzi huu utakapokamilika  utapunguza  tatizo la msongamano wa watumishi  katika  idara  mbalimbali, uwepo wa ukumbi wa mikutano  ambapo  kwa sasa  mikutano yote muhimu ikiwemo  vikao vya  waheshimiwa  madiwani  hufanyika  katika  darasa  la shule ya Msingi Buhigwe. Kazi zilizotekelezwa  hadi  sasa  ni  Kufyatua tofali, Kuchimba msingi wa jengo.,Kumwaga zege la blinding, Kumwaga zege la msingi na Kujenga kuta hadi usawa wa lenta. Changamoto zilizopo ni pamoja na Ukosefu wa maji eneo la mradi, Ukosefu wa vifaa vya ujenzi kama mchanga na kokoto ambavyo vinatoka Kigoma Mjini karibu Km 80.,Gharama kubwa za vifaa vya viwandani mfano, saruji 50 kg. niTsh.18,000/= na Ukosefu wa umeme.Serikali  inaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi.                                   Mradi huu  mpaka  utakapokamilika   awamu ya kwanza utakuwa umegharimu  jumla ya Tsh  1,156,262,213 ( Serikali kuu Tsh ,1,148,462,213 na Halmashauri Tsh 7,800,000/=.)
    Mkimbiza mwenge kitaifa ndg Amour Hamad Amour, akiweka jiwe la msingi kwenye ofisi za mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe.
  4.  Klabu ya kupinga dawa za Kulevya-Shule ya Sekondari Buyenzi. Kikundi hiki cha kupinga na kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya kimeanzishwa  tarehe 18 mwezi  Mei 2017chenye  jumla ya wananchama  sitini  (60) ambao ni wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Buyenzi.Shule hii  ni ya kutwa yenye kitado cha kwanza hadi cha nne  na  ni shule yenye mchanganyiko wa jinsi. Lengo la kikundi hiki ni kupinga matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana na jamii  kwa ujumla  ikiwa ni pamoja  na Kutoa ushauri kwa watumiaji wa madawa ya  kulevya, Kuwa mabalozi kwa vijana wenzao kuhusiana na kupinga matumizi ya madawa ya kulevya kwa namna ya kumsaidia mtumiaji  wa  madawa ya kulevya ili aache kutumia.Kutoa elimu kwa kuwajengea uwezo wakutambua madhara yatokanayo na matumizi ya madawa ya kulevya. Kujenga uwezo wanafunzi namna ya kujizuia au kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya. Pia kutambua adhabu kwa watu wanaojishughulisha na madawa ya kulevya. Kuelimisha jamii juu ya madhara na athari za matumizi ya madawa ya kulevya na kutoa ushauri kwa wanaotumia madawa ya kulevya. Uhaba wa vitendea kazi kama vipeperushi vya kutosha vinavyohusiana na madawa ya kulevya, limu, n.k, Hakuna ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na  hakuna fedha kwa ajili ya kuendesha huduma hii.
    Ndg Amour Hamad Amour akipokea risala toka kwa mwanafunzi wa sekondari Buyenzi kabla ya kuzindua klabu yao ya upingaji dawa za kulevya.
  5. Ujenzi wa  Jengo la Utawala  ,Vyoo na Madarasa  Shule ya Msingi  Muyama. Shule ya msingi Muyama ilianzishwa mwaka  1954. Shule hii ina wanafunzi 662, walimu 10, nyumba za walimu 8 na vyumba vya madarasa 6.
    Mradi huu unajumuisha ujenzi wa  jengo la utawala, ujenzi wa vyumba vitatu (3) vya madarasa , ukarabati wa vyumba sita (06)  na ujenzi wa matundu sita (06)  ya choo. Aidha mradi huu ulianza tarehe 16/02/2017 na  kukamilika tarehe 15/07/2017.Lengo kuu la mradi huu ni  kuboresha mazingira ya ufundishaji kutokana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa awali  na  darasa la kwanza ,uhaba wa ofisi za utawala na uhaba wa matundu ya choo.Aidha  ujenzi na uboreshaji wa miundombinu hii itaongeza ufanisi katika kutoa elimu bora kwa kuzingatia uwiano wa mwanafunzi na miundombinu iliyopo. Kazi zilizotekelezwa katika ujenzi wa matundu sita ya choo, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, jengo la utawala na ukarabati wa vyumba sita vya madarasa  ni kuchimba shimo la choo ,kufyatua matofali, kusomba mawe, kukusanya kokoto na mchanga na kusomba , kujenga shimo la choo, kufunika choo , kujenga  ukuta wa choo na kupaua , kujenga  vyumba vya madarasa sita , kujenga jengo la utawala  na  ukarabati wa vyumba sita vya madarasa.Mradi huu umegharimu jumla ya Tsh. 133,200,000ambapo serikali kuu imechangia Tsh 111,000,000 na nguvu za wananchi  thamani ya Tsh 22,200,000.
    Ndg Amour Hamad Amour akiweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa jengo la utawala, vyoo na madarasa shule ya msingi Muyama
  6. Matengenezo  ya barabara ya Kitambuka –Mnanila Herimission. Barabara ya Munanila-Kitambuka yenye urefu wa kilomita 4.2 inaunganisha Kijiji cha Musagara na Kitambuka. Katika barabara hii kulikuwa kuna kipande cha kilomita 3.0 ambazo zilikuwa ni korofi na kutopitika hasa kipindi cha masika kutokana na utelezi. Hivyo Halmashauri iliiweka kwenye mpango wa matengenezo maalum wa kilomita 4.2 ambapo kati ya hizo kilomita 03 ziliwekwa kifusi.Matengenezo haya maalum ya kilomita 4.2 cha barabara ya Munanila-Kitambuka yalianza 27/09/2016 na kumalizika 28/12/2016. Lengo  la  matengenezo maalum ya kilomita 4.2 ni  kuboresha  huduma ya usafiri  na mawasiliano kwa kuwezesha   vyombo vya usafiri  na waenda kwa miguu kuweza kufanya shughuli za kimaendeleo  pamoja na kuepusha ajali zisizo za lazima.Kazi zilizotekelezwa katika barabara hii kwa kipande cha 4,2 km ni pamoja na Upanuzi wa barabara kutoka mita 4.0 mpaka upana wa mita 5.0,  Uchongaji wa barabara kwa kilomita 4.2,  Uwekaji wa changarawe kilomita 3.0 , kuzibua mitaro/mifereji iliyoziba  na  Kufungua mifereji mipya. Mradi huu umegharimu kiasi cha Tsh. 62,582,000   kutoka Mfuko wa Barabara.
    Barabara ya Munanila-Kitambuka, ikizinduliwa rasmi na Ndg Amour Hamad Amour (Mkimbiza mwenge kitaifa)
     
  7. Ujenzi wa wodi ya Akina Mama na  Watoto  zahanati  ya Kitambuka. Ujenzi wa zahanati ya Kitambuka upo katika kata ya Mkatanga yenye jumla ya wakazi  19,241 katika kijiji cha Kitambuka. Aidha zahanati hii ina jumla ya watumishi wane (4) akiwemo Tabibnu Msaididi mmoja, Muuguzi mmoja, na wahudumu wa afya wawili. Lengo la mradi huu  ni kutoa huduma za afya ya uzazi kwa akina mama  wajawazito waliopo katika kijiji cha Kitambuka na kata ya Mkatanga kwa ujumla.Jengo hili litaweza kutoa huduma ziafuatazo  kulingana na sehemu za jengo:- chumba cha kujifungulia, chumba cha kusubiria kabla ya kujifungua, chumba  cha kupumzika baada ya kujifungua, na sehemu ya huduma ya kliniki ya baba, mama na mtoto. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa Msingi, Kuta, Kupaua na  umaliziaji wa jengo (Usafi wa Jengo). Gharama ya mradi huu umegharimu kiasi  cha  Tsh 89,400,000 (Mchango wa  wananchi   Tsh 2,400,000/= na  Wahisania  ni  Tsh87,000,000).
    Uzinduzi wa zahanati ya Kitambuka kwa ajili ya mama, wajawazito na watoto ikizinduliwa na Ndg Amour Hamad Amour

0 comments:

Post a Comment