Tuesday, 1 August 2017

MBIO ZA MWENGE WILAYANI BUHIGWE 2017

                 Mbio za mwenge wa uhuru wilaya  ya Buhigwe kwa mwaka 2017 zilifanyika tarehe   27-28/07/2017   wilayani hapa, ambapo Jumla ya miradi saba (7) yenye thamani ya shilingi.1,946,132,975 imetembelewa na mwenge wa uhuru mwaka huu 2017 na kuzinduliwa/kuweka jiwe la msingi.
Ndg Frederick Joseph Ndahani (mkimbiza mwenge kitaifa) akikimbia na mwenge wa uhuru  Kata ya Kinazi wilayani Buhigwe  


 Aidha, Serikali kuu imechangia shilingi 1,819,532,975 sawa na 94% Halmashauri shilingi 14,200,000 sawa na 1%, Wahisani shilingi 87,000,000 sawa na 4% na Wananchi shilingi 25,400,000 sawa na 1% katika kufanikisha uzinduliwaji wa miradi hiyo.

Mbali na uzinduzi wa miradi hiyo, mbio za mwenge kwa mwaka 2017 zilibeba jumbe nne (4) kuu kuwafikishia wananchi


  • "MADAWA YA KULEVYA" Mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, tuwajali na kuwasikilize watoto na vijana.
  • "RUSHWA" Tuungane kwa pamoja dhidi ya rushwa kwa maendeleo, amani na usalama wa Taifa letu.
  • "UKIMWI" Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI inawezekana ifikapo mwaka 20130
  • "MALARIA" Shiriki kutokomeza Malaria kabisa kwa manufaa ya jamii.
Miradi ambayo mwenge wa uhuru kwa mwaka 2017 ilizindua wilayani Buhigwe ni kama ifuatavyo:
  1. Mradi  wa maji Katika kijiji cha Kirungu. Ujenzi wa miundo mbinu ya Maji ya  bomba katika Kijiji cha Kirungu unaendelea kujengwa na  Mkandarasi mjenzi  KAM / JUVE CONSTRUCTION LTD, ukisimamiwa na wataalamu wa maji toka ofisi ya mhandisi wa maji Wilaya ya Kasulu na Buhigwe. Lengo kuu la Mradi ni kuwapatia wananchi wa Kirungu  huduma ya maji safi na salama na ya kutosha kwa umbali  usiozidi mita  400 toka majumbani mwao kwa kuzingatia sera ya maji ya mwaka 2002, kwa kufanya hivyo wananchi  watapata muda wa ziada wa kufanya kazi nyingine za uzalishaji  mali na kujiletea maendeleo. Katika  mradi huu kazi zifuatazo  zimefanyika; ujenzi wa chanzo cha maji umekamilika kwa asilimia 95 , ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye  mita za ujazo 150m3 unaendelea na umefikia asilimia 85, njia kuu ya bomba (4,081m)  imekamilika kwa  asilimia 85,njia za mitawanyo kijijini (5,709m) imekamilika kwa  asilimia  90 na Vituo vya kutekea maji 15 (double type taps) vimejengwa na kukamilika kwa  asilimia  80. Mradi wa maji wa Kijiji cha Kirungu utakapokamilika utagharimu kiasi cha Tshs 504,788,762 (Wananchi  Tsh3,200,000/=, Halmashauri Tsh 4,000,000/= na Serikali kuu Tsh 497,588,762)mpaka kufika hatua hii mkandarasi ameishalipwa kiasi cha Tshs 412,839,702.20 na chanzo cha fedha hii  ni serikali kuu.
    Ndg Amour Hamad Amour akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji kijiji cha KIRUNGU
     
  2. Klabu ya Wapinga  rushwa  -Shule ya Sekondari  ya  Saint  Mathias Mulumba. Klabu  ya wapinga rushwa ya shule ya Sekondari Saint Matius  imeanzishwa mwaka 1994 ikiwa ni sera ya Serikali ya kuwajenga vijana kimaadili. Klabu hii ina jumla ya wanachama 40 waliojiunga kwa hiari yao wenyewe na wamepewa mafunzo kuhusu maana ya rushwa, aina za rushwa, sababu na madhara ya rushwa kwa Taifa letu. Klabu hii ni miongoni  mwa klabu kumi na tisa (19) za  shule za msingi na sekondari ambazo zimeshaanzishwa katika Wilaya ya Buhigwe. Lengo kuu la kuanzishwa klabu hii  ni  kuelimisha jamii kuhusu maana ya rushwa,  madhara  na umuhimu wa kuzuia na kupambana na rushwa. Wanafunzi wataelimisha jamii kwa njia ya midahalo, michoro, nyimbo, ngonjera, mashairi, maigizo na makala ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU. Kazi zinazotekelezwa ni kutoa mafunzo kwa Vijana kwani ni rasilimali muhimu katika kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuwa ni  wepesi wa kujifunza na kubadilika. Wakishirikishwa ipasavyo katika mapambano dhidi ya rushwa tutajenga jamii ya Watanzania waadilifu ambao wataichukia rushwa na maovu yote na hivyo kuleta maendeleo. Hili litakuwa suluhisho la uhakika na la kudumu katika kuikabili rushwa kwani mmomonyoko wa maadili ni moja ya sababu za msingi za kuwepo kwa rushwa katika jamii.
    Ndg Amour Hamad Amour, azidindua mradi wa wapinga rushwa katika shule ya sekondari ya mtakatifu Mathius Mulumba iliyopo Janda
  3. Ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya  Buhigwe. Ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi  makao makuu  Wilaya ya Buhigwe umeanza mwaka 2015  ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwa  na ofisi  za utawala  katika makao  makuu ya wilaya

    Halmashauri imepokea kiasi cha Tsh 1,200,000,000/= (Tsh 450,000,000/= kwa mwaka 2014/15 na Tsh 750,000,000/= kwa mwaka 2016/17) kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu. Mradi huu unatekelezwa naTanzania  Building  Agency  (TBA)  ambayo ni taasisi ya Serikali. Lengo kuu la mradi  huu  ni   kuboresha mazingira ya kiutendaji kazi  ya  kiutawala   na   kitaalamu. Aidha, Ujenzi huu utakapokamilika  utapunguza  tatizo la msongamano wa watumishi  katika  idara  mbalimbali, uwepo wa ukumbi wa mikutano  ambapo  kwa sasa  mikutano yote muhimu ikiwemo  vikao vya  waheshimiwa  madiwani  hufanyika  katika  darasa  la shule ya Msingi Buhigwe. Kazi zilizotekelezwa  hadi  sasa  ni  Kufyatua tofali, Kuchimba msingi wa jengo.,Kumwaga zege la blinding, Kumwaga zege la msingi na Kujenga kuta hadi usawa wa lenta. Changamoto zilizopo ni pamoja na Ukosefu wa maji eneo la mradi, Ukosefu wa vifaa vya ujenzi kama mchanga na kokoto ambavyo vinatoka Kigoma Mjini karibu Km 80.,Gharama kubwa za vifaa vya viwandani mfano, saruji 50 kg. niTsh.18,000/= na Ukosefu wa umeme.Serikali  inaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi.                                   Mradi huu  mpaka  utakapokamilika   awamu ya kwanza utakuwa umegharimu  jumla ya Tsh  1,156,262,213 ( Serikali kuu Tsh ,1,148,462,213 na Halmashauri Tsh 7,800,000/=.)
    Mkimbiza mwenge kitaifa ndg Amour Hamad Amour, akiweka jiwe la msingi kwenye ofisi za mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe.
  4.  Klabu ya kupinga dawa za Kulevya-Shule ya Sekondari Buyenzi. Kikundi hiki cha kupinga na kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya kimeanzishwa  tarehe 18 mwezi  Mei 2017chenye  jumla ya wananchama  sitini  (60) ambao ni wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Buyenzi.Shule hii  ni ya kutwa yenye kitado cha kwanza hadi cha nne  na  ni shule yenye mchanganyiko wa jinsi. Lengo la kikundi hiki ni kupinga matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana na jamii  kwa ujumla  ikiwa ni pamoja  na Kutoa ushauri kwa watumiaji wa madawa ya  kulevya, Kuwa mabalozi kwa vijana wenzao kuhusiana na kupinga matumizi ya madawa ya kulevya kwa namna ya kumsaidia mtumiaji  wa  madawa ya kulevya ili aache kutumia.Kutoa elimu kwa kuwajengea uwezo wakutambua madhara yatokanayo na matumizi ya madawa ya kulevya. Kujenga uwezo wanafunzi namna ya kujizuia au kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya. Pia kutambua adhabu kwa watu wanaojishughulisha na madawa ya kulevya. Kuelimisha jamii juu ya madhara na athari za matumizi ya madawa ya kulevya na kutoa ushauri kwa wanaotumia madawa ya kulevya. Uhaba wa vitendea kazi kama vipeperushi vya kutosha vinavyohusiana na madawa ya kulevya, limu, n.k, Hakuna ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na  hakuna fedha kwa ajili ya kuendesha huduma hii.
    Ndg Amour Hamad Amour akipokea risala toka kwa mwanafunzi wa sekondari Buyenzi kabla ya kuzindua klabu yao ya upingaji dawa za kulevya.
  5. Ujenzi wa  Jengo la Utawala  ,Vyoo na Madarasa  Shule ya Msingi  Muyama. Shule ya msingi Muyama ilianzishwa mwaka  1954. Shule hii ina wanafunzi 662, walimu 10, nyumba za walimu 8 na vyumba vya madarasa 6.
    Mradi huu unajumuisha ujenzi wa  jengo la utawala, ujenzi wa vyumba vitatu (3) vya madarasa , ukarabati wa vyumba sita (06)  na ujenzi wa matundu sita (06)  ya choo. Aidha mradi huu ulianza tarehe 16/02/2017 na  kukamilika tarehe 15/07/2017.Lengo kuu la mradi huu ni  kuboresha mazingira ya ufundishaji kutokana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa awali  na  darasa la kwanza ,uhaba wa ofisi za utawala na uhaba wa matundu ya choo.Aidha  ujenzi na uboreshaji wa miundombinu hii itaongeza ufanisi katika kutoa elimu bora kwa kuzingatia uwiano wa mwanafunzi na miundombinu iliyopo. Kazi zilizotekelezwa katika ujenzi wa matundu sita ya choo, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, jengo la utawala na ukarabati wa vyumba sita vya madarasa  ni kuchimba shimo la choo ,kufyatua matofali, kusomba mawe, kukusanya kokoto na mchanga na kusomba , kujenga shimo la choo, kufunika choo , kujenga  ukuta wa choo na kupaua , kujenga  vyumba vya madarasa sita , kujenga jengo la utawala  na  ukarabati wa vyumba sita vya madarasa.Mradi huu umegharimu jumla ya Tsh. 133,200,000ambapo serikali kuu imechangia Tsh 111,000,000 na nguvu za wananchi  thamani ya Tsh 22,200,000.
    Ndg Amour Hamad Amour akiweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa jengo la utawala, vyoo na madarasa shule ya msingi Muyama
  6. Matengenezo  ya barabara ya Kitambuka –Mnanila Herimission. Barabara ya Munanila-Kitambuka yenye urefu wa kilomita 4.2 inaunganisha Kijiji cha Musagara na Kitambuka. Katika barabara hii kulikuwa kuna kipande cha kilomita 3.0 ambazo zilikuwa ni korofi na kutopitika hasa kipindi cha masika kutokana na utelezi. Hivyo Halmashauri iliiweka kwenye mpango wa matengenezo maalum wa kilomita 4.2 ambapo kati ya hizo kilomita 03 ziliwekwa kifusi.Matengenezo haya maalum ya kilomita 4.2 cha barabara ya Munanila-Kitambuka yalianza 27/09/2016 na kumalizika 28/12/2016. Lengo  la  matengenezo maalum ya kilomita 4.2 ni  kuboresha  huduma ya usafiri  na mawasiliano kwa kuwezesha   vyombo vya usafiri  na waenda kwa miguu kuweza kufanya shughuli za kimaendeleo  pamoja na kuepusha ajali zisizo za lazima.Kazi zilizotekelezwa katika barabara hii kwa kipande cha 4,2 km ni pamoja na Upanuzi wa barabara kutoka mita 4.0 mpaka upana wa mita 5.0,  Uchongaji wa barabara kwa kilomita 4.2,  Uwekaji wa changarawe kilomita 3.0 , kuzibua mitaro/mifereji iliyoziba  na  Kufungua mifereji mipya. Mradi huu umegharimu kiasi cha Tsh. 62,582,000   kutoka Mfuko wa Barabara.
    Barabara ya Munanila-Kitambuka, ikizinduliwa rasmi na Ndg Amour Hamad Amour (Mkimbiza mwenge kitaifa)
     
  7. Ujenzi wa wodi ya Akina Mama na  Watoto  zahanati  ya Kitambuka. Ujenzi wa zahanati ya Kitambuka upo katika kata ya Mkatanga yenye jumla ya wakazi  19,241 katika kijiji cha Kitambuka. Aidha zahanati hii ina jumla ya watumishi wane (4) akiwemo Tabibnu Msaididi mmoja, Muuguzi mmoja, na wahudumu wa afya wawili. Lengo la mradi huu  ni kutoa huduma za afya ya uzazi kwa akina mama  wajawazito waliopo katika kijiji cha Kitambuka na kata ya Mkatanga kwa ujumla.Jengo hili litaweza kutoa huduma ziafuatazo  kulingana na sehemu za jengo:- chumba cha kujifungulia, chumba cha kusubiria kabla ya kujifungua, chumba  cha kupumzika baada ya kujifungua, na sehemu ya huduma ya kliniki ya baba, mama na mtoto. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa Msingi, Kuta, Kupaua na  umaliziaji wa jengo (Usafi wa Jengo). Gharama ya mradi huu umegharimu kiasi  cha  Tsh 89,400,000 (Mchango wa  wananchi   Tsh 2,400,000/= na  Wahisania  ni  Tsh87,000,000).
    Uzinduzi wa zahanati ya Kitambuka kwa ajili ya mama, wajawazito na watoto ikizinduliwa na Ndg Amour Hamad Amour

Tuesday, 18 July 2017

UZINDUZI WA BENKI YA MATOFALI KATA YA MUNZEZE

UZINDUZI WA BENKI YA MATOFALI KWA AJILI YA UJENZI WA KITUO CHA AFYA KATA YA MUNZEZE WILAYA YA BUHIGWE.
Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe imezindua benki ya matofali kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Munzeze. uzinduzi huo umefanyika julai 14, 2017 na kuhudhuriwa na afisa tawala wa wilaya Bw Peter Masindi (kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bhigwe), mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Bw Anosta Nyamoga, OCD wa wilaya Bw Venance Mapala na mwenyeji wao mheshimiwa Wilson Luzibira (Diwani wa kata hiyo).
Uzinduzi huo ambao ulikadiriwa kuwa na lengo la kufyatua tofali elfu kumi (10,000) kwa ajili ya umaliziaji wa kituo hicho cha afya. Viongozi hao wa wilaya wamliwasihi wananchi waendelee na moyo wa kujitowa kuleta maendeleo yao wenyewe na kuwakumbusha kuwa serikali ipo nao kukamilisha juhudi zao hizo. Zaidi ya hayo, viongozi hao wa wilaya walitoa rai kwa wananchi wa wilaya hiyo kuiga mfano wa kuigwa wa wananchi wa kata ya Munzeze kwa kile walichokifanya siku hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Bw Anosta Nyamoga akishirikiana na wananchi wa kata ya Munzeze kuandaa udongo kwa ajili ya kufyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Munzeze


Wananchi wa kata ya Munzeze wilayani Buhigwe wakionesha ari yao katika siku ya uzinduzi wa benki ya matofali kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata yao.

Baadhi ya wanakamati ya ulinzi na usalama, akishiriki kwenye zoezi zima la ufyatuaji wa matofali katika siku ya uzinduzi wa benki ya matofali kata ya Munzeze

Jengo la kituo cha afya kata ya Munzeze ambalo wananchi wamejitokeza kufyatua tofali kuendeleza ukamilishaji wa jengo hilo







Sunday, 15 January 2017

UZINDUZI WA MAZOEZI KWA MATUMISHI WA UMMA KATIKA HALMASHAURI YA BUHIGWE



"Mazoezi ni afya"
 Kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe mkoa Kigoma, siku ya Jumamosi (14.01.2017) ilizindua rasmi mazoezi kwa watumishi wa Halmashauri. "Lengo kuu ya mazoezi hayo nijenga mwili na kujiepusha na magonjwa yasio ambukiza, kama vile ugonjwa wa presha ya damu, kuongezeka uzito niongoni mwatatizo kubwa kwa wengi mwa watumishi wa umma, kupitia mazoezi hayo ambayo yanataraji kufanyika kila jumamosi ya wiki ya pili ya mwezi"

Mkuu wa wilaya akataja faida zipatikanazo kwa kufanya mazoezi.
1. Mazoezi ya mwili husaidia kulirekebisha shinikizo la Damu.
2.  Mazoezi ya Mwili huiruhusu damu nyingi zaidi kuzifikia sehemu zote za mwili na kuifanya mikono na miguu ipate joto.
3. Mazoezi ya mwili yanaondoa mambo yote ya mwili, yaani mkazo wa mwili na mfashaiko wa moyo na kukusaidia wewe kujisikia vizuri zaidi katika maisha yako. Mazoezi ni tiba bora.
4. Mazoezi ya mwili hujenga afya yako
5. Mazoezi ya mwili huimarisha misuli pia nakunawirisha mwili kwa ujumla
6. Mazoezi huongeza ufanisi makazini

Mkuu wa wilaya alisema maneno yaho katika ufunguzi wa mazoezi kisha akayaongoza kwakukimbia umbali wa Kilometa 6 kutoka ofisi za Halmashauri ya Wilaya Buhigwe.


Kanali Marco Gaguti (Mkuu wa wilaya ya Buhigwe) Kulia mwa picha. Akitowa meneno ya ufunguzi wa mazoezi hyo


Namkurugenzi wa Halmashauri pia alishiriki kikamilifu ili kuhamashisha nawengine kufanya mazoezi hayo.
Nd. Anost Nyamoga (Kushoto mwa picha) Mkurugenzi wa Halmashauri akiwa akipasha misuli moto kabla ya kuanza kukimbia mbio za Kilometa 6
 Michezo ilipatikana baada ya kukimbia umbali ya Kilometa 6, ni kama ifuatayo:-
i. Kukimbiza kuku kwa wafanya kazi wa Halmashauri pamoja na MDs
ii. Mbio za maguni
iii. Kupiga pushapu kwa MDs na kwa watumishi wenye uwezo wakufanya hivyo.

Mazoezi yote hayo yaliongozwa na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya Mwenye, Kama katika picha zinavyoonesha.

Yafuatayo ni matukio kwa njia ya picha kwa kila mazoezi.

Mkuu wa Wilaya Akiongoza MDs katika Mbio za Kilometa 6 Wakifuatiwa na Watumishi wa Halmashauri.

Nd. Bakena (DT wa Halmashauri Buhigwe) ni miongoni mwa washiriki wa mbio hizo.


Watumishi wa Halmashauri wakiwa katika ushiri wao wa mazoezi


Matembezi ya Kilometa 6 kwa watumishi

Mkuu wa Kitengo Cha Ugavi na Manunuzi (PMU) Kusho mwa picha  Nd. Magengele pamoja na Fundi umeme wa Halmashauri Bw. John Kaboto
Add caption

Pushapu kwa baadhi ya Md na Watumishi walioweza kufanya hivyo wakisimamiwa na Mkuu wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya akiwa anaongoza mazoezi hayo baada ya kumaliza mbio za kilometa 6

Mshindi wa mbio za Kuku. Akiwa ameshikilia zawadi yake.

Mbio za Magunia kwa Wanawake

Mbio za Maguni kwa wazee umri kati ya 50-55




Wednesday, 19 October 2016

KIKAO CHA KWANZA CHA BARAZA LA BIASHARA BUHIGWE

           
Kwa awamu ya kwanza, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ilifanikiwa kufanya kikao cha kwanza cha baraza la biashara Octoba 18, 2016 kilichodhaminiwa na Local Goverment Climate (LiC)
             Kikao hicho kilichofanyika Wilayani hapa na kuhudhuriwa na mwenyekiti wake Kanali Marco Gaguti (Mkuu wa wilaya ya Buhigwe), akiambatana na katibu wa baraza hilo (Kaimu Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Buhigwe Ndg Sadock Kihuriko), pamoja na wawakilishi wa LiC mkoa wa Kigoma, wawakilishi kutoka sekta mbalimbali na wajumbe wa baraza hilo.
             Kikao hicho kilijadili agenda kuu nne

  1. Elimu ya biashara na ujasiliamali (Business and entrepreneurship Training).
  2. uwezekano wa kuboresha/mikakati ya kusaidia uwekezaji (access to finance/investment support stratergies).
  3. mikakati ya mwelekeo wa vipaumbele vya minyororo ya thamani (Stratergic direction for priority).
Mwenyekiti wa kikao cha baraza la biashara (Kanali Marco Gaguti) akifungua rasmi kikao hicho na kutoa maelezo na umuhimu wa baraza hilo hasa katika kuonesha fursa, changamoto na hata mikakati ya nini kifanyike ili kunufaika na uwepo wa baraza hilo katika kuleta manufaa ya wanabuhigwe kwa ujumla na kuboresha mapato ya Halmashauri kwa kupitia fursa za biashara.
"Mazingira Bora ya biashara kwa kukuza mapato ya ndani ya  Halmashauri"
Katikati ni mwenyekiti wa baraza Kanali Marco Gaguti, kulia kwake  Katibu wa baraza la biashara Kaimu mkurugenzi Ndg Sadock Kihuriko na kushoto kwake mwenyekiti wa TCCIA wilaya ya Buhigwe Ndg Azaria Kalobho.

Baada ya ufunguzi wa Mwenyekiti wa Baraza hilo, akatoa  fursa kwa wajumbe wa baraza hilo kuanza kujadili agenda za kikao hicho. Katika kujadili agenda za kikao, Mwenyekiti aliomba wajumbe na wawakilishi kutoka sekta binafsi kutoa japo historia ya soko la Nyamugali angalau kwa wajumbe kujuwa umuhimu wa soko hilo katika kumnufaisha mwanainchi mfanyabiashara na hata Halmashauri katika kuongeza mapato yake. 
Bwana Paul Bahinda  mwakilishi kutoka Buhigwe Green Innovation (BGI), akitoa historia ya soko hilo na faida zake kwa watumiaji na nini kifanyike katika kuboresha soko ili lengo la kumnufaisha mfanyabiashara litimie na hata mapato ya Halmashauri pia. (Picha hapo chini)




Katika mjadala huu ilibidi meneja wa LiC mkoa wa Kigoma Dr Betty Mlingi (Pichani chini) kutoa ufafanuzi wa namna LiC inavyojitokeza kusaidia baadhi ya miradi ambayo inakuwa imeshafanyiwa tathmini na ufuatiliaji wa karibu wa mradi husika. Na baada ya hapo ndipo LiC yajitokeza kuunga mkono kufanisha mradi huo.


Katika agenda hiyo, mwenyekiti alishauri azimio litolewe na andiko liandikwe na kazi ya soko hilo ifanyike. Zaidi ya yote mwenyekiti wa baraza Kanali Marco Gaguti (pichani chini) alitia nia ya kuchukua dhamira kulifanikisha hilo akishirikiana na mkurugenzi wa Halmashauri na wadau kutoka sekta mbalimbali ya kitu gani kifanyike.



Agenda ziliendelea kujadiliwa na hapa ndipo suala la kukopesheka likajadiliwa kama moja ya agenda kikaoni.
Katibu wa baraza, Ndg Saddock Kihuriko (Kaimu mkurugenzi wa wilaya katika baraza) akikaribisha agenda ya uwezekano wa kukopesheka.

Agenda hii ilibeba na hoja ya kutopatikana kwa benki katika wilaya na hivyo kufanya wafanyabiashara kupata taabu ya namna ya ubebaji wa fedha zao hasa wakati wa kwenda kwenye magulio na hata kuhatarisha maisha yao.
Akielezea suala hilo kikaoni, afisa mikopo wa benki ya NMB Kasulu, Bw. Kulwa Shotto (Pichani chini) alilihakikishia baraza kuwa benki hiyo imepata nafasi wilayani kwa ajili ya kujenga tawi dogo na kuanza kutoa huduma hiyo ifikapo mwezi wa Disemba mwaka huu.
Zaidi ya yote, afisa mikopo huyo aliwaondoa wasiwasi wana baraza hilo kwa niaba ya wajasiliamali wengine kuwa NMB wapo kuwakopesha wafanyabiashara kwa ajili ya kufanikisha malengo yao kibiashara.




Baadhi ya wajumbe wa baraza kutoka sekta tofauti wakisikiliza agenda ya mikopo kutoka mwakilishi wa NMB Kasulu


Agenda ya Mikakati ya mwelekeo wa vipaumbele vya minyororo ya thamani, ilijadiliwa. katika agenda hii suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kutokuwepo kwa viwanda kwa ajili ya usindikaji wa mazao yaliyo uti wa mgongo wilayani yalidaliwa na zaidi ya yote uboreshwaji wa mnada wa wilaya na majosho.

Ndg Boniface Nanda (Afisa kilimo wilaya) akifafanua suala la pembejeo na uwepo wa viwanda vya usindikaji mazo yapatikanayo katika wilaya yetu na hata namna ya kupata mitambo ya kufanyia kazi hiyo.

Ndg Keneth Tefurukwa (Afisa mifugo wilaya) akitoa ufafauzi kwa baraza juu ya suala la uboreshwaji wa mnada wa wilaya na majosho.


Katika kikao hicho, wajumbe na wadau waliguswa na agenda zilizoandaliwa na mafisa biashara wa wilaya na hivyo kuwafanya washiriki vilivyo katika kikao.
Ndg Philemon Home ( mdau kutoka taasisi binafsi) akichangia agenda ya kilimo, hasa katika upatikanaji wa pembejeo na mifugo katika majosho na mnada  

Katika suala la kilimo ambamo jamii kubwa inajihusisha kwa ujumla, suala la upatikana wa pembejeo kwa bei nafuu na hata kupata mitambo/mashine za usindikaji wa baadhi ya mazao yalimwayo wilayani hapa, mdau Ayubu Fidel (sekta binafsi) hakusita kuzungumzia umuhimu na uhitaji wa vitu hivyo kwa wakulima wa wilaya ya Buhigwe mbele ya mwenyekiti Kanali Marco Gaguti na balaza lake kwa ujumla.

Ndg Ayubu Fidel Chanko (Mdau sekta binafsi)


Suala la ukamilishwaji wa ujenzi wa kituo cha biashara (one stop business centre) nalo halikuachwa kama mengineyo katika kikao hicho na aliyewakilisha sekta binafsi wilaya ya Buhigwe Ndg Venance Kigwinya, akashauri baraza kwa kupitia usimamizi wa mwenyekiti wake kukamilisha utafiti na hata ujenzi wa kituo hicho ifikapo Januari 2017 kama ilivyoahidiwa na meneja wa LiC mkoa wa Kigoma Dr Betty Mlingi.

Ndg Venance Kigwinya, akifafanua juu ya umuhimu wa kituo hicho cha biashara kilivyo na tija kwa wafanya biashara wa wilaya ya Buhigwe

Kwa mamlaka aliyonayo, mwenyekiti wa baraza kabla ya kufunga kikao alitoa nafasi kwa wageni toka nje ya wilaya ya Buhigwe kutoa japo neno kuhusu mjadala wa agenda za siku hiyo na ndipo Ndg Francis Peter (kutoka LiC Dodoma) akatoa hongera zake kwa mwenyekiti (Mkuu wa wilaya ya Buhigwe) Kanali Marco Gaguti kwa kuwa na timu nzuri iliyoonesha uchu na nia ya kuyatekeleza yote yaliyojadiliwa ili kutoa matunda bora kwa jamii. Mwakilishi huyo hakusita kupongeza namna agenda zilivyoandaliwa na zaidi ya yote kujali muda zaidi katika kujadili hoja hizo

Ndg Francis Peter (Akiwakilisha LiC Dodoma)


Akihitimisha na kufanga kikao mwenyekiti wa baraza la biashara la wilaya ya Buhigwe Kanali Marco Gaguti alitoa shukrani zake kwa wageni kutoka LiC na hata wale walioalikwa kutoka sekta tofautitofauti na zaidi yayote wajumbe wa baraza hilo na kufunga kikao hicho rasmi.



Mwenyekiti wa baraza la biashara la wilaya ya Buhigwe Kanali Marco Gaguti akifunga kikao cha kwanza cha baraza la biashara wilaya ya Buhigwe



Mwenyekiti wa baraza la biashara akiwa katika picha ya pamoja na wageni na wajumbe wa baraza zima la biashara la wilaya ya Buhigwe.

Mwenyekiti Kanali Marco Gaguti (katikati walioketi ), kutoka kushoto kwake ni meneja wa LiC mkoa wa Kigoma Dr Betty Mlingi mwenyekiti wa TCCIA wilaya ya Buhigwe Ndg Azaria Kalobho kulia kwake  Katibu wa baraza la biashara Kaimu mkurugenzi Ndg Sadock Kihuriko na Katibu tawala wilaya ya Buhigwe Ndg Peter Masindi,